Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa, Manji amezungumza na wachezaji hao uso kwa uso na kuwaambia Sh milioni 100 ni mali yao kama watatimiza anachotaka.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kuwa, Manji amewaambia wachezaji hao kwamba anachotaka ni kushinda mechi zote tano (kabla ya juzi) zilizobaki za ligi ikiwemo ile ya Simba.
“Mechi ya kwanza ilikuwa ni dhidi ya Oljoro, ni kama vile wachezaji wameshaanza kumla ng’ombe. Maana wameshinda mechi moja na zimebaki nne,” kilieleza chanzo cha uhakika.
“Hii si hadithi, Manji mwenyewe alikuja kambini na kuzungumza na wachezaji na kuwaambia nia yake hiyo. Lakini kitu kizuri zaidi, dau hilo la shilingi milioni mia linaweza kuzidi kwa kuwa amewaambia katika mechi dhidi ya Simba atatoa ahadi mpya.
“Maana yake wanatakiwa kushinda mechi nne zilizobaki kwanza, maana tukishinda mechi tatu, tayari sisi ni mabingwa. Lakini Manji amesema anataka ushindi wa mechi zote tano.
“Wachezaji wanalijua hilo na umeona juhudi zimeanza katika mechi ya kwanza dhidi ya Oljoro. Lakini kikosi kiko vizuri, mimi ninaamini watashinda mechi zote zilizobaki.”
Taarifa zinaeleza kuwa, huenda Manji akaongeza dau hadi kufikia Sh milioni 150 watakapokutana na Simba Mei 18 katika mechi ya mwisho ya ligi hiyo.
Manji amewaambia wachezaji wa Yanga kuwa, anataka wachukue ubingwa, lakini hautanoga bila ya kuifunga Simba ambayo msimu uliopita iliwatwanga mabao 5-0 halafu ikachukua na ubingwa.
Recent Comments