MCHEZAJI kiraka kwenye kikosi cha Simba, Shomari Kapombe amesema dalili zinaonyesha kuwa hata kuipata nafasi ya pili au ya tatu ni jambo gumu, lakini nguvu zao wanaelekeza kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizosalia katika Ligi Kuu ya Bara.
Simba sasa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36, ambazo ni nne nyuma ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya tatu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kapombe ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza kwa bidii msimu huu, alisisitiza kuwa ni jambo gumu pia hata kushika nafasi ya tatu ambayo kwao ilionekana kuwa rahisi kuipata baada ya kushushwa kileleni na Yanga.
“Mimi siku zote si mtu wa kukata tamaa, nitapambana hadi mwisho, lakini nadhani sasa mambo yamekuwa magumu zaidi, hata hiyo nafasi ya tatu tunaweza tusiipate,” alisema Kapombe.
Kapombe ambaye ni kati ya wachezaji chipukizi Simba, amekuwa mmoja wa mabeki tegemeo wa kikosi hicho msimu huu.