KOCHA Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amemwambia kiungo mchezeshaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, kwamba atakuwa amefanya kosa kubwa kama akiondoka Msimbazi.
Kauli hiyo ya Julio inakuja wakati Ngassa akiwa anaelekea kumaliza muda wake wa kuichezea Simba kwa mkopo mwishoni mwa msimu huu. Pia atakuwa amemaliza mkataba na Azam FC inayommiliki.
Ngassa amekuwa akiripotiwa kuwa tayari ameshasaini mkataba na Yanga, lakini amewahi kukanusha suala hilo mbele ya viongozi wa Simba.
Lakini Julio amemwambia anatakiwa ahakikishe anabaki Msimbazi, kwani anaweza kupata mafanikio zaidi akiwa klabuni hapo kuliko katika kikosi kingine chochote hapa nchini.
Julio alisema Ngassa ana nafasi kubwa ya kupata maendeleo makubwa endapo atabaki Simba, kutokana na sera ya timu hiyo kutokuwa na kigugumizi juu ya kuuza nyota wake nje ya nchi kwa fedha nyingi kuliko timu yoyote hapa nchini.
“Sioni sababu ya Ngassa kurudi Yanga wala Azam, huko kote alishacheza na hakuna jipya alilopata, Simba ndiyo timu pekee ambayo itamfanya apate mafanikio zaidi kwa hapa nchini.
“Najua jukumu la kuamua hatima ya maisha yake anayo yeye mwenyewe, lakini namshauri kama mwanangu, ikiwa anataka mafanikio zaidi kuliko ilivyo sasa anatakiwa kubaki hapa ambapo patamrahisishia mengi au kama akishindwa basi aende nje ya Tanzania,” alisema Julio.